MWENYEKITI
wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amewataka wanachama
wake kuacha unyonge na kujibu mapigo ya wapinzani hasa wale ambao wanaendesha
siasa za vurugu katika kampeni za chaguzi mbalimbali nchini.
Rais Kikwete
amesema kuwa uvumilivu una ukomo, na kwamba sasa wanachama wa CCM hawana budi
kuacha unyonge, kutokana na siasa hizo za vurugu zinazoendeshwa na vyama vya
upinzani.
Aliyasema
hayo jana mjini hapa wakati akifungua kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC) ya CCM kitakachokutana kwa siku mbili chini ya uenyekiti wake,
ambacho ajenda kuu ni kuzungumzia Bunge Maalumu la Katiba.
“Tumelizungumzia
hili katika Kamati Kuu, tumekubaliana kuacha unyonge (makofi). Ndio watu
wamelisema hili katika Kamati Kuu, tumesema jamani tumekubaliana kuacha
unyonge,” alisema Rais Kikwete ambaye wakati anafungua kikao hicho waandishi wa
habari walikuwamo, na akaongeza: “Wacha wakaseme (waandishi wa habari), ndio
tumekubaliana kuacha unyonge. Kabisa. Hata kama leo katika taarifa za habari,
zisiwekwe habari nyingine, msikike ninyi tu. Uvumilivu una ukomo wake.”
Mwenyekiti
huyo wa CCM alisema wamefikia hatua hiyo kwa sababu yanayotokea yanasikitisha
sana na akatoa mfano wa matukio kadhaa ya uvunjifu wa amani katika kampeni
katika maeneo ya Igunga mkoani Tabora na Kahama mkoani Shinyanga.
“Maana
tunashindana na wenzetu wagomvi maana wao ugomvi ndio sehemu ya mwongozo wa
kufanya kazi ya siasa. Maana pale Kahama kijana wamemtoa macho kwa bisibisi.
Acheni unyonge (makofi). “Nasema kwa kweli kwa sababu yanayotokea
yanasikitisha. Pale Igunga kijana yule wamemmwagia tindikali, pale Kahama
kijana wamemtoa macho kwa bisibisi. Tuache unyonge,” alisisitiza Rais Kikwete
huku akishinikizwa kwa shangwe za CCM Oyee, Mapinduzi Daima.
Ingawa Rais
Kikwete hakutaja chama, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekuwa
kikihusishwa na vurugu za uchaguzi katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya Igunga
na Kahama katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika hivi karibuni na pia
katika chaguzi ndogo za ubunge.
Pongezi za
ushindi
Akizungumzia
uchaguzi mdogo wa kata 27 zilizofanyika hivi karibuni na CCM kuzoa kata 23,
Rais Kikwete aliwapongeza wanaCCM kwa ushindi huo, lakini akawapa changamoto ya
kuhakikisha wanarejesha kata hizo nne zilizokwenda kwa vyama vya upinzani.
“Huu ni
ushindi mkubwa sana, ushindi mnono. Ni vizuri kutumia nafasi hii kujipongeza na
kuwapongeza wenzetu kwa kazi nzuri, kazi nzuri waliyoifanya ya kujenga chama,”
alisema Rais Kikwete na kuongeza: “Lakini tukumbushane kwamba kata nne
hatukuzipata, hivyo tuna kazi ya kuzikomboa, sisi wakati wote nia yetu ni
kushinda, kushindwa haiwezekani.”
Aidha,
alizungumzia uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, akisema hadi
sasa hali ni shwari, hakuna migawanyiko wala misukosuko kama ilivyokuwa kwa
Jimbo la Arumeru Mashariki ambalo alisema tangu mwanzo hadi mwisho, hali
haikuwa shwari.
Alisema hadi
sasa wana uhakika wa ushindi katika jimbo hilo, lakini akawataka wanaCCM
kujiandaa vyema kwa kila hali na kuhakikisha ushindi unapatikana katika jimbo
lililoachwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William
Mgimwa.
Mwanawe
Geoffrey ndiye mgombea wa CCM. Pia aliwataka wanachama na viongozi wa Jimbo la
Chalinze mkoani Pwani, nao kujiandaa kwa uchaguzi mdogo kwa sababu tayari Spika
wa Bunge, ametoa taarifa serikalini kuhusu kuwa wazi kwa jimbo hilo kutokana na
kifo cha mbunge wake, Said Bwanamdogo.
“Msikae tu
kusubiri na kuendelea kuomboleza, kwa sababu Serikali haiombolezi, wao
wanachotaka ni uchaguzi ujazwe, shughuli ziendelee. Maana watu wanaweza kusema
hata orobaini bado. Kule Arumeru tuliambiwa tumbo bado halijapasuka. Kwani kwa
Mgimwa orobaini tayari, mbona mchakato umeanza. “Ninyi fanyeni mchakato,
orobaini yetu mnaweza kufanya wakati mambo mengine yakiendelea. Tujiandae
mapema ili kuhakikisha tunashinda,” alisema Mwenyekiti huyo wa CCM na
kuwapongeza viongozi wa mkoa na wilaya waliofanikisha ushindi katika uchaguzi
mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki ambako mgombea wao, Mahmoud Thabit Kombo
alishinda.
Alisema CCM
ilibidi kumtosa aliyekuwa mbunge wao, Mansour Yussuf Himid, kwa sababu alikuwa
akivaa magwanda ya chama hicho, lakini alikuwa akipinga sera na taratibu za
chama hicho tawala.
“Kila
akifungua mdomo wake anaitukana CCM, kila akifungua mdomo anapingana na sera za
CCM. Tukasema inatosha, bora kuwa na mpinzani huko nje kuliko huyu, ndio maana
niliwahi kusema katika NEC moja hapa kuwa sijui mtu anasema nitahama CCM,
nikasema nendeni sasa hivi,” alisema Kikwete.