Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa
mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, Mheshimiwa William
Mgimwa, aliyekuwa pia Mbunge wa Jimbo la Kalenga (Mkoa wa Iringa) kupitia Chama
cha Mapinduzi (CCM).
Rais Kikwete
amesema kuwa taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi lilipokuwa
linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa ambao amekuwa akiutoa kupitia
nafasi zake za Waziri wa Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la
Kalenga.
Kifo cha Mheshimiwa
Mgimwa kimetangazwa mchana wa leo, Jumatano, Januari Mosi, 2014, na Katibu Mkuu
Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Sefue kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Katika
tangazo lake, Balozi Sefue amesema kuwa Waziri Mgimwa ameaga dunia asubuhi ya
leo saa 5:20 (Saa za Afrika ya Kati) katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic ,
Pretoria, Afrika Kusini ambako amekuwa amelazwa kwa muda sasa.
Balozi Sefue
amesema kuwa maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa Waziri Mgimwa
yanafanywa na Serikali kwa kushirikiana na familia yake na kuwa taarifa zaidi
za suala hilo zitatolewa baadaye kwa kadri zinavyopatikana na maandalizi
yanavyoendelea.
Katika
salamu zake kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda na kwa familia ya Marehemu
Mgimwa, Rais Kikwete amesema: “Sina
maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia taarifa za
kifo cha Mheshimiwa Mgimwa.
Binafsi
nimemtembelea mara mbili kwenye Hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho
hali yake ilikuwa imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi
akanielezea nia yake na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake
ilikuwa nzuri.”
Ameongeza
Mheshimiwa Rais Kikwete: “Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote
tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu.”
“Napenda
kutoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana-familia wote kwa
kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa.
Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni majonzi
yangu,” amesema Rais Kikwete.
Rais pia
amewatumia rambirambi wananchi wa Jimbo la Kalenga akisema kuwa wamempoteza
mwakilishi na mtetezi mahiri wa maslahi yao.
Mgimwa
aliyezaliwa January 20, 1950 na kuwa mbunge wa jimbo la Kalenga mkoani Iringa
kupitia chama cha Mapinduzi (CCM)
Dk. Mgimwa
alikuwa mkufunzi katika Chuo cha Benki mkoani Mwanza, kabla ya kufanikiwa
kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mkoa wa Iringa, katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2010.