
KWAKO, Emmanuel Mgaya ‘Masanja’. Naamini u mzima na unaendelea
vyema na majukumu yako ya kila siku. Kwa upande wangu nipo sawa, nakimbizana na
maisha.
Nina machache ya kukushauri kuhusiana na maisha yako kama staa ambaye kwa sasa
umetangaza kuokoka. Kwa maneno mengine ni kwamba, umeondoka kwenye utaifa, upo
mikononi mwa Muumba wako.Nimekufahamu kwa kitambo kidogo. Kwangu mimi, wewe ni
mmoja wa mastaa wa ukweli katika uchekeshaji Bongo. Mwenye kipaji cha hali ya
juu na unayejua unachokifanya.
Tatizo ni kwamba, nashangazwa na aina ya maisha yako baada ya kutangaza
kuokoka. Ninavyojua mimi, kuokoka ni kuachana na maisha ya awali ambayo
(pengine) yalikuwa hayampendezi Mola na kugeukia katika maisha safi.Niliposikia
umeokoka nilifurahi kuona kuwa umeelekea sehemu sahihi zaidi kiimani. Lakini
moyoni nilikuwa na shaka kidogo maana wapo wasanii wengi kwenye uigizaji ambao
walitangaza kuokoka lakini baadaye wakaonekana kwenye njia zao za awali.
Ukiachana na waigizaji, pia kuna wasanii wa Bongo Fleva ambao nao waliingia
kwenye ulokole na mara wakaamua kurudia maisha yao ya awali.Baadaye
nikasikia kuwa unasomea Uchungaji (ingawa inaelezwa kuwa ni Uinjilisti), hapo
sikuwa na shaka tena na wokovu wako. Niliamini kwa mtu ambaye ameamua kuingia
kwenye kufundisha wengine njia iliyo sahihi hawezi kudanganya kuwa ameokoka.
Siyo kama naingilia maisha yako au nakukosoa kwenye suala la imani yako. Uzuri
ni kwamba, nami ninaamini katika imani yako, hivyo sioni tatizo
kukushauri.Tatizo lipo kwenye staili yako ya maisha. Ni kweli kwamba umeokoka,
lakini itawezekana vipi usuke mabutu kichwani? Maandiko yanaeleza wazi kuwa,
wanaoamini ni barua inayosomeka kwa watu wote.
Je, watu watasoma nini kupitia mabutu? Unaweza kusema kuwa, imani ya mtu iko
moyoni, hapo sitakubaliana na wewe, maana kinachoonekana nje, kinawakilisha
kilichomo ndani.Vipi kama kanisa zima, wanaume wataingia wamesuka?
Nafikiri si jambo sahihi. Watu watapata shaka na wokovu wako, tena mchunga
kondoo. Wengine wanaweza kuona wokovu si jambo ‘serious’. Kwamba mtu anaweza
kuingia na akaendelea na mambo yake yaleyale, jambo ambalo si la kweli.
Wokovu ni pamoja na mwonekano wa nje. Mavazi, mitindo ya nywele n.k.Jambo
jingine ambalo limenishangaza ni namna unavyoingiza komedi kwenye mambo yanayohusu
dini.Usahihi wa kufanya utani kwenye vichekesho huku ukitaja jina la Mungu
unatokea wapi? Masanja tumezuiwa kufanya mzaha au kulitaja bure Jina la Mungu
wetu.
Nakushauri kama ni kweli umeamua kuokoka, badilika lakini kama unahisi bado
unatamani maisha ya kawaida na kujichanganya, chagua moja ili jamii
isikutafsiri tofauti.Ni uamuzi wako kufuata au kuacha hapahapa, lakini la
muhimu ni kwamba, nitakuwa nimeshakushauri. Ubarikiwe sana mpendwa!
Yuleyule,
Mkweli daima,
.........................
Joseph Shaluwa.