Polisi wanne
wamekamatwa kuhusiana na kisa cha kuwapiga risasi waandamanaji nchini Afrika
Kusini siku ya Alhamisi.
Tshepo
Babuseng, mwenye umri wa miaka 28, alipigwa risasi na polisi katika maandamano
kuhusu swala la makaazi viungani mwa mji wa Johannesburg.
Ripoti za
awali, zilisema kuwa umati wa watu uliwavamia polisi waliokuwa wanaondoa vifusi
barabarani. Hapo ndipo polisi mmoja alipowapiga risasi waandamanaji hao.
Mmoja wa
maafisa hao anakabiliwa na tuhuma za mauaji wakati wengine wakikabiliwa na kosa
la ukandamizaji.
Msemaji wa
polisi katika mkoa wa Gauteng, amesema kuwa polisi hao walio na umri wa kati ya
miaka 33-49 watafikishwa mahakamani hivi karibuni.
Kitengo cha
kuchunguza polisi kinasema kuwa kitafanya uchunguzi huru wa ndani kuhusiana na
tuhuma hizo.
Kwa sasa
polisi hao wameachishwa kazi kwa muda hadi kesi itakapoamuliwa.
Polisi
nchini Afrika Kusini hutuhumiwa mara kwa mara kuhusu kuwatesa watu na kutumia
njia zisizofaa kupambana na makundi ya watu wanaokuwa wanaandamana.
Mapema wiki
hii kufuatia hatua ya polisi kuwapiga risasi watu wanne katika maandamano
tofauti, waziri wa polisi Nathi Mthethwa aliambia BBC kuwa polisi watakawaua
raia wasio na hatia hawatalindwa.
"polisi
wanapata mafunzo kuwalinda raia na kuwahudumua. Hawafunzwi kuwaua,'' alisema
waziri huyo.
Mwaka 2012,
polisi waliwapiga risasi wafanyakazi 34 wa migodi waliokuwa wanagoma katika
mgodi wa Marikana , tukio la kushangaza zaidi kuwahi kutokea tangu kumalizika
kwa enzi ya ubaguzi wa rangi 1994.
Mwaka jana
maafisa walinaswa kwa kanda ya video wakimfunga mwanamume kwenye gari kabla ya
kumburura barabarani. Mwanamume huyo alipatikana akiwa amefariki.
0 comments:
Post a Comment