WAKATI Watanzania wakilia ugumu wa maisha pamoja na mambo
mengine, kupanda kwa gharama za nishati ya umeme, imethibitishwa kuwa kuna
wafanyabiashara wanapambana bei hiyo isishuke. Wafanyabiashara hao; wenye
mitambo ya kufua umeme wa mafuta na waagizaji wa mafuta, wananufaika kwa
kunyonya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambalo linalazimika kuwapa karibu
Sh bilioni nne kila siku, ili lipate umeme huo wa mafuta kutoka kwao.
Akizungumza juzi katika siku ya mwisho ya ziara yake
ya kutembelea ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kuchakata gesi Mtwara na
Lindi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema wafanyabiashara hao wanauzia Tanesco
umeme uniti moja kwa kati ya senti 33 na 50 ya dola ya Marekani.
Bei hiyo ya umeme kwa Tanesco ni kubwa kuliko ambayo
shirika hilo linauza kwa wateja wanaotumia umeme mdogo wa majumbani, wa kati
kwa wafanyabiashara, wa kati viwandani na mkubwa kwa viwanda vikubwa, na kubwa
kuliko bei ya umeme ya mashirika ya umeme ya nchi za Afrika Mashariki.
Tanzania kwa sasa inatumia megawati 1,850 ambazo
asilimia 80 kwa mujibu wa Pinda, zinazalishwa kwa mafuta ya dizeli na mazito;
wakati asilimia nyingine ndizo zinazotokana na vyanzo vingine vya maji na gesi
ya Songosongo.
Bei ya umeme Kwa mujibu wa takwimu za Tanesco, wateja
majumbani wananunua uniti moja kwa senti 19 ya dola, wateja wa biashara senti
13 na viwanda vya kati na vikubwa senti 10. Umeme wa taa za barabarani ni senti
19.
Kwa nchi za Afrika Mashariki, hasa Kenya, Uganda na
Rwanda, wateja majumbani hununua uniti moja kwa senti 20, wa biashara ni kati
ya senti 16 na 20.
Viwanda vya kati Uganda bei ni senti 17, Kenya 14 na
Rwanda 19. Kwa umeme wa viwanda vikubwa, bei kwa Uganda ni senti 12, Kenya 15
na Rwanda 19. Tanzania inaongoza kwa kutoza bei kubwa kwa taa za barabarani
ambayo ni senti 19 sawa na Rwanda huku Kenya na Uganda bei kwa umeme huo ni
senti 18.
Hali hiyo inadhihirisha kuwa pamoja na kupandisha bei
ya umeme mwezi huu, bado gharama za umeme kwa Tanesco ni kubwa kuliko bei ya
kuuzia, na kusababisha shirika hilo muhimu katika uchumi wa nchi, kujiendesha
kwa hasara.
Suluhisho Pinda alisema bomba la gesi kutoka Mtwara
likimalizika kujengwa na uzalishaji kuanza, Tanesco itanunua umeme huo kwa
senti 8 na kufanya nishati hiyo kushuka bei. Kauli hiyo ya kushusha bei ya
umeme baada ya gesi kuanza kutumika Dar es Salaam, pia ilipata kutolewa na
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
“Hii bei ya umeme iliyopo sasa ni ya muda tu na
itashuka sana bomba la gesi litakapokamilika, kwa sababu hata mitambo ya kufua
umeme inayotumia mafuta nayo itatumia gesi na mitambo mipya ya gesi italetwa,
nataka Watanzania wakubali hivyo.
“Serikali inataka umeme mwingi utokane na gesi, jua,
upepo na joto ardhi, lakini wapo wanaokataa bomba kuja Dar es Salaam na hao hao
wanalalamika umeme kuwa juu, mtu yeyote ambaye anajua dunia inakwendaje, hawezi
kupinga kujengwa bomba la gesi.
"Miaka ijayo, chanzo kikubwa cha umeme nchini
kitakuwa gesi asilia… nyie mtanitukana, mtanisema sana, lakini mimi nitabaki
kwenye utaalamu na wala siwezi kuyumba, tatizo la umeme wa Tanzania
litatatuliwa na gesi, kila kitu kikikamilika Tanesco na Ewura (Mamlaka ya
Udhibiti wa Nishati na Maji) hawawezi kuendelea kuweka bei juu," alisema
Profesa Muhongo.
Mapambano “Sisi tunaona kuwa suluhu ya kuondokana na
gharama hizi ni gesi, lakini kuna watu wanajua watanyang’anywa tonge midomoni,
vita hii tunaijua; lakini hatuwezi kurudi nyuma katika hili ni lazima tusonge
mbele,” alisema Pinda.
Alisema nyuma ya mapambano ya kuzuia gesi kufika Dar
es Salaam, wapo wafanyabiashara ambao wanahofia kuwa mwisho wa biashara yao ya
kuuzia Tanesco umeme kwa bei ya juu umefika.
Alisema watu kwa sasa wananufaika na Tanesco kununua
mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme. Katika hali hiyo, Pinda alisema uamuzi
wa Serikali kuchimba gesi hiyo na kuisafirisha hadi Dar es Salaam si jambo
jepesi, kwani utekelezaji wake unakabiliwa na mapambano na upinzani mkubwa
kutoka kwa wenye mitambo ya kuzalisha umeme ambao kwa sasa wananufaika kutoka
Tanesco.
Alisisitiza, kuwa Serikali imedhamiria kuachana na
umeme huo wa mafuta na kama wafanyabiashara hao wanataka kuendelea na biashara
hiyo, ni vema wabadilishe mitambo yao iwe ya gesi na si ya mafuta kama ilivyo
sasa.
Mataifa, ushauri Pia alisema vita nyingine
wanayokabiliana nayo ni ya nchi ambako kampuni za utafiti wa mafuta na gesi
zinatoka, ambazo zinataka kampuni zao zipewe zabuni ya kutandaza bomba la gesi
na kujenga mitambo ya kuchakata gesi.
“Wanalalamika gesi wametafuta na kugundua wao, halafu
kandarasi anapewa China, sisi tumewajibu kuwa tumekimbilia China kwa sababu
masharti yao ni nafuu kuliko yao,” alisema Pinda.
Katika hatua nyingine, Pinda alitaka wakazi wa Lindi
na Mtwara kutambua kuwa gesi hiyo ni rasilimali ya Taifa na itanufaisha nchi
nzima. Aliwataka wajiandae kwa uchumi huo kwa kuhakikisha wanatumia fursa
zilizopo kufaidika. Aliwataka wasikubali fursa ya gesi ilete balaa nchini
badala ya neema.
“Kama tunataka iwe neema tushirikiane na wadau wakubwa
zaidi ili nchi yetu ipige hatua kimaendeleo.”
Kwa upande wake, Profesa Muhongo aliwataka wananchi wa
mikoa ya Lindi na Mtwara kusomesha watoto wao hasa katika Sayansi, ili
wafaidike na uwepo wa gesi na mafuta katika mikoa hiyo.
Alisema Serikali imejitahidi kusomesha vijana katika
eneo la gesi na wamekuwa wanahamasisha vijana wa mikoa hiyo kuchukua masomo ya
Sayansi kwa vile wizara inagharimia baadhi ya vijana kusoma masuala ya gesi
vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi.
Pinda katika ziara hiyo alielezea kuridhika na kazi
inayoendelea katika mradi huo na akasema upo uwezekano mradi huo ukakamilika
kabla ya muda wake uliopangwa wa miezi 18.
0 comments:
Post a Comment