Marekani imefungia kituo cha ndege zisizo na rubani nchini
Ethiopia ambacho imekuwa ikitumia kushambulia wanamgambo wa al-Shabab katika
taifa jirani la Somalia.
Maafisa wa Marekani wanasema kituo hicho cha siri kilikuwa
cha muda tu na kwamba kwa sasa hakikihitajiki tena.
Kirasmi, Marekani ina kambi moja tu ya jeshi barani Afrika,
ambayo imepewa jina Camp Lemonnier nchini Djibouti. Lakini huwa ina kambi
nyingi za muda maeneo mengi barani.
Oktoba mwaka 2015, jarida la habari za ufichuzi The
Intercept, lilichapisha nyaraka za siri za jeshi ambazo lilisema lilionyesha
Marekani ilikuwa na kambi zaidi ya 14 za ndege zisizo na rubani barani Afrika.
Ndege hizo zimetumiwa kuua makamanda kadha wa al-Shabab,
akiwemo kiongozi wa kundi hilo Ahmed Godane mwaka 2014.
Wakosoaji wanasema mashambulio hayo huwa hayapati shabaha
wakati wote na mara nyingine huua watu wasio na hatia.
Vyombo vya habari Ethiopia vinasema Marekani ilianza kutumia
kituo hicho kilichoko kusini mwa nchi hiyo 2011.
Ethiopia imekuwa mshirika wa karibu wa Marekani katika vita
dhidi ya al-Shabab, na pia imekuwa na wanajeshi Somalia tangu 2006.
0 comments:
Post a Comment