MICHAKATO

Levis Rocky Ndekeno

This is default featured slide 1 title

Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.

This is default featured slide 2 title

Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.

This is default featured slide 3 title

Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.

This is default featured slide 4 title

Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.

This is default featured slide 5 title

Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.

Pages

Sunday, February 2, 2014

WAUMINI wa Kanisa la Break Through Assemblies lililoko eneo la Boko Magengeni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam linadaiwa kuuza Sakramenti kwa Sh 100,000 kwa kila muumini. Hatua hiyo inadaiwa kuwanyima wasio na fedha chakula hicho cha Bwana hivyo kusababisha malalamiko dhidi ya uongozi wa Kanisa hilo la Walokole.

Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili, zilisema tukio hilo lililoshangaza waumini lilitokea Januari 19. Kanisa hilo linaongozwa na Mchungaji Godfrey Simtomvu.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, na kwa masharti ya kutotajwa majina, waumini walisema kitendo hicho kiliwashangaza siku hiyo kanisani hapo walikokuwa wamekwenda kwa ajili ya Ibada kama siku zingine.

Akisimulia, mmoja wao alisema baada ya Mchungaji kuhubiri, vililetwa vikombe na mikate ambayo hutumiwa kanisani kama ishara ya kushiriki pamoja Chakula cha Bwana. Makanisa mengine hutambua ibada hiyo kama ya Sakramenti ya Chakula cha Bwana.

“Baada ya vifaa hivyo kufika kanisani hapo vilionekana kuwa vichache tofauti na waumini waliokuwa kanisani hapo…ndipo Mchungaji alipopaza sauti kuwa mwenye Sh 100,000 na zaidi ndiye atakayeshiriki,” alisema na kuongeza kuwa Januari 26, alishindwa kuabudu kutokana na kitendo hicho.

Alisema baada ya kutamka hivyo, waumini wengi walinywea wakashindwa kusogea na kupisha watu wapatao 10; lakini baada ya kuona idadi imekuwa ndogo zaidi ikatangazwa kuwa hata wenye Sh 50,000 wanaweza kusogea mbele kushiriki.

Aliongeza kuwa wakati wote huo waumini walikuwa wakitazamana, wakijiuliza juu ya utaratibu huo mpya, jambo ambalo ni kinyume na ilivyokuwa awali kanisani.

Alisema Mchungaji baada ya kuona idadi ya waumini inazidi kupungua, akawatangazia kuwa wasiokuwa na fedha wajiandikishe kisha wapokee chakula hicho kisha na kesho yake wapeleke kiwango hicho cha fedha. Muumini mwingine alisema jambo lililoshangaza wengi ni utaratibu huo mpya ambao awali haukuwapo kwani walikuwa wakitangaziwa wiki moja kabla na kutakiwa kujitayarisha kwa ajili ya ibada hiyo ya Chakula cha Bwana.

“Awali Mchungaji alikuwa akitupa taarifa wiki moja kabla, akiwataka waumini kujitayarisha na kusafisha nyoyo zao kabla ya kushiriki kitendo hicho ambacho tuliamini kuwa ni kitakatifu na chenye mafundisho makubwa kwa waumini,” alisema na kuongeza kuwa hilo la kununua chakula lilizuka ghafla na hakujua hatma yake.

Mwingine alisema mbali na kununua chakula hicho, pia jambo lililozusha mshangao kwa waumini ni Mchungaji huyo kuleta watu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuhubiri Neno la Mungu akidai kuwa ni wahubiri ambao nao husisitiza neno la kutoa tu.

“Waumini tunaamini kuwa Bwana Yesu alitoa chakula hicho bure…iweje leo waumini wauziwe tena kwa kupangiwa kiwango?” Alihoji.

Akizungumzia madai hayo, Mzee wa Kanisa hilo alisisitiza kuwa yeye si msemaji wa Kanisa hilo na kusema madai hayo hayana ukweli na kwamba siku hiyo, Mchungaji hakumaanisha kwamba utakuwa utaratibu, bali ilikuwa ni kuhamasisha utoaji kwa muumini mwenye nacho. Alisema kufanya hivyo halikuwa lengo la kutafuta fedha bali kupeleka Neno la Mungu mbele.

“Msemaji wa Kanisa ni Mchungaji mwenyewe, ukiniuliza sana mimi utakuwa unanionea, kama unamtafuta na ukamkosa atakuwa redioni katika kipindi,” alisema mzee huyo.

Akizungumzia malalamiko hayo, Mchungaji Simtomvu alisema kutokea kwa hali hiyo si imani ya Kanisa hilo bali ilitokana na mhubiri kutoka Kongo ambaye alifunuliwa na Mungu na kutaka waumini kuweka maagano yao na Mungu kwa mwaka huu.

Alisema hayo yalikuwa mafunuo ya mtu na si imani na ni kitu ambacho hutokea mara moja tu na kutolea mfano wa yai linapouzwa kwenye mnada kwa bei kubwa, ingawa bei yake halisi inajulikana.

“Laiti ningemfahamu aliyeleta taarifa hiyo ningemsaidia, kwani amekengeuka, mbona Mchungaji TB Joshua wa Nigeria huuza maji katika vichupa vidogo kwa gharama kubwa inayoweza kufikia Sh 75,000,” alisema Mchungaji Simtomvu.


Alisema tukio hilo ilikuwa ni kwa muumini anayetaka kuweka agano na Mungu wake, kwamba mwaka huu amtendee mambo gani na kuhoji kuwa zipo imani za ajabu ajabu lakini haziripotiwi.

Saturday, February 1, 2014

Japan kujenga reli iliyobomolewa na mafuriko Morogoro

Makamu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mitsuya Norio (Kushoto), akiwa na Naibu waziri wa uchukuzi, Dk. Charles Tizeba, wakati walipotembelea miundombinu ya reli jijini Dsm jana.



Serikali ya Japan imeahidi kukarabati kipande cha reli kinachosumbua mara kwa mara kilichoko kati ya Kilosa na Dodoma.

Hayo yalielezwa jana na Naibu Waziri wa Uchukuzi Dk. Charles Tizeba, wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Norio Mitsuya, aliyetembelea bandari ya Dar es Salaam na kampuni ya reli (TRL) kujionea uendeshaji.

Ziara hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, alizotoa wakati wa ziara ya Afrika ili kuisaidia sekta ya miundombinu.
Alisema baada ya waziri huyo kujionea shughuli mbalimbali, kwa niaba ya serikali yake ameahidi kuisaidia Tanzania kuimarisha reli na bandari.

Aliongeza kuwa juzi kampuni hodhi ya miundombinu ya reli (Rahco) na TRL zilifanya tathmini ya eneo la Kilosa hadi Dodoma ambapo serikali hiyo iliahidi kulikarabati.
Aliongeza kuwa, baada ya ukarabati huo Japan itasaidia kuitengeneza rasmi ambapo gharama yake itajulikana pale tathmini itakapofanyika. Alisema nia ya kuisaidia Tanzania kwenye usafiri wa reli ni ya muda mrefu na kwamba kwa sasa wanatimiza ahadi hiyo.

Kuhusu bandari ya Dar es Salaam, alisema Japan itaipanua kwa kutengeneza gati namba moja hadi saba. Waziri Mitsuya alisema lengo la ziara hiyo ni kuisaidia Tanzania katika kuboresha miundombinu kwa siku zijazo.

Awali, Waziri Tizeba alisema kuwa, vichwa 13 vya treni ambavyo wameviagiza nchini Marekani hivi karibuni vinatarajia kuingia mwishoni mwa mwaka huu. Aliongeza vichwa hivyo vinagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 50.
Katika ziara hiyo, waziri wa Japan alipata nafasi ya kusafiri na treni ya Dar es Salaam kutoka stesheni hadi Ubungo.

Pinda: Tanzania itanufaika na uwekezaji ikizingatia mfumo wa uwekezaji

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika katika masuala ya uwekezaji endapo itatekeleza mapitio ya mfumo wa uwekezaji yaliyoandaliwa na taasisi ya washirika walioendelea kiuchumi.

Pinda aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaa wakati akizindua taarifa ya uwekezaji.
Alisema malengo ya mapitio ya mfumo huo ni kuboresha hali ya uwekezaji na biashara ambayo matokeo yake yatasaidia kuongeza wawekezaji katika maeneo mengi.

“Kuna maeneo ya uwekezaji yanayopata mitaji kutoka nje FDI ambayo ni umeme, mafuta, gesi, madini, viwanda, ujenzi na huduma za jamii.” 

Alisema matokeo ya jitihada hizo ni makubwa na yameonekana ndani ya miaka miwili baada ya utafiti wa ripoti hiyo kufanyika.

Alitolea mfano kilimo ambacho kimekua kutoka Dola za Marekani milioni 304.5 mwaka 2010 hadi Dola milioni 355.4 mwaka 2011.
Pia alisema katika sekta ya umeme na gesi zimekua kutoka Dola milioni 328.6 hadi 539.8 mwaka 2011.

Pinda alisema hali hiyo imesababisha pato la taifa kuendelea kukua kwa asilimia sita kwa miaka kumi mfululizo ambapo kwa mwaka jana lilikua kwa asilimia saba na matarajio ni kufikia asilimia 7.2 kwa mwaka huu. 

Miongoni mwa maeneo yanayohusishwa na mfumo huu wa mapitio ya Uwekezaji ni yale yaliyoainishwa katika Matokeo Makubwa Sasa ambayo ni Kilimo, Maji, Uchukuzi, Elimu na Nishati. 

Aliomba wadau wote kwa kushirikiana na Sekta binafsi kuchambua kwa makini mapendekezo ya mapitio ya mfumo huo ambayo yanatumika pia kuharakisha mafanikio ya Matokeo Makubwa Sasa.

Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi ya OECD, Bw. Rintaro Tamaki, alisema mazingira ya uwekezaji nchini yanabadilika kila mara kutokana na kuvumbuliwa kwa rasilimali mpya kama vile gesi, makaa ya mawe ambazo zinasababisha watu wavutiwe kuwekeza 
Aliitaka serikali kutozipuuza sekta kama ya kilimo na kueleza kuwa kinachotakiwa ni kuiboresha kwa kuanzisha viwanda ili kuongeza thamani ya mazao yenu. 

Wednesday, January 29, 2014

Msanii wa Nigeria KCEE, adaiwa kulipa tshs mil 675 kufanya collabo na Nicki Minaj

Kama ulishangaa kusikia kuwa Diamond Platnumz alilipa dola 5,000 ili kumshirikisha Davido kwenye remix ya My Number One, huenda ukaishiwa nguvu kusikia kiwango kinachodaiwa kutolewa na msanii wa Nigeria, KCEE ili kufanya collabo na first lady wa YMCMB, Nicki Minaj.


Kuna tetesi kuwa KCEE amelipa kitita cha N68m, ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 675 za Tanzania ili amshirikishe malkia huyo mpya wa hip hop nchini Marekani. Kufuatia tetesi hiyo, meneja wa KCEE, Soso Sobrekon, ameongea na mtandao wa NET kufafanua mambo yalivyo.
“Tupo nchini Marekani kujaribu kupata collaboration. Ni kweli tupo kwenye mchakato wa kufanya wimbo na Nicki Minaj. Tulitaka kuifanya iwe surprise kwa mashabiki lakini kwakuwa tayari imejulikana, tunataka kuifanya iwe kuwa zaidi,” alisema.
Hata hivyo meneja huyo alikataa kuthibitisha kama kweli kiwango hicho ndicho walicholipa. “Tunataka kumuongeza msanii mwingine wa YMCMB ambaye ni mkubwa kuliko Nicki Minaj. Nicki ameshathibitishwa kuwa kwenye wimbo huo, lakini kwakuwa sasa kila mtu anafahamu, bado tutawasurprise mashabiki kwa kumchukua msanii mwingine kutoka YMCMB.’

Monday, January 27, 2014

JK aagiza JWTZ kujenga kambi ya muda Kilosa

RAIS Jakaya Kikwete, ameagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kujenga kambi ya muda ya mahema na mabati katika kijiji cha Magole mkoani Morogoro, ili waathirika wote wa mafuriko wasio na nyumba, waishi kwenye kambi hiyo. Mbali na agizo hilo, pia ameitaka Serikali kuandaa utaratibu wa kupata magodoro kutoka katika kampuni zinazotengeneza magodoro hayo na kuwagawia waathirika hao.
Ametoa maagizo hayo jana katika viwanja vya Shule ya Sekondari Magole, ambako kumewekwa kambi ya muda kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea Januari 22, mwaka huu.
Akiwa katika kambi hiyo, Rais Kikwete aliyewasili jana mchana kwa helkopta ya Polisi, alishuhudia idadi kubwa ya waathirika waliokumbwa na mafuriko wakiwemo watoto wadogo, wakilala chini na kuwa hatarini kupatwa na magonjwa ya vichomi na kuhara.
Kabla ya kutembelea waathirika na kuwahutubia, Rais Kikwete alitembelea daraja lililoathirika na mafuriko, maeneo yaliyoathirika vibaya na kupewa taarifa ya athari ya mafuriko kwa kata za Wilaya ya Kilosa, Gairo na Mvomero.
“Mafuriko haya ni makubwa na hayajawahi kutokea , watu wameathiriwa kwa nyumba zao kubomoka, kujaa maji na kuwafanya kukosa makazi na wengi wao wanalala chini.
“Serikali itatafuta magodoro kati ya siku mbili hizi na kuyaleta hapa kwa waathirika wa mafuriko ili kila mmoja alale kwenye godoro na si chini, lengo ni kuwaepusha kupatwa na magonjwa hasa ya vichomi na kwa watoto kuhara.
“Wenye viwanda hivi vya magodogo waendelee kuzalisha kwa wingi na waliyokuwa nayo stoo walete …hatuwezi kuwaacha watu waendelee kulala chini,” alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wa chakula, alisema Serikali inacho cha kutosha kwenye maghala yake ambayo aliagiza yafunguliwe na chakula hususani maharage na mahindi, yasambazwe kwa waathirika.
Aliomba pia wadau wengine waendelee kujitokeza kusaidia kutoa chakula hasa mchele. Kuhusu huduma ya maji, alisema itaendelea kutolewa na magari ya JWTZ, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na magari ya kampuni za ujenzi za China hadi huduma ya maji kwenye kijiji hicho na vingine itakapotengemaa.
Pia alizungumzia umuhimu wa kuwatafutia waathirika na wakazi wengine, maeneo mengine ya miiinuko yenye usalama kwa kujenga makazi yao ya kudumu.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amewataka wakuu wa wilaya za Mkoa wa Morogoro pamoja na wakurugenzi watendaji wa halmashauri, kuwahudumia wananchi nyakati za matatizo, kwani uongozi wao utapimwa na wananchi kutokana na ushiriki wao wa moja kwa moja kwao.
Ametoa kauli hiyo, baada ya kutoridhishwa na takwimu za waathirika wa mafuriko zilizotolewa na uongozi wa Mkoa, kuhusu idadi ya kaya na watu waliokumbwa na mafuriko katika tarafa ya Magole, Wilaya ya Kilosa; Dakawa Wilaya ya Mvomero na Gairo kutoonesha mchanganuo halisia.
Kutokana na kasoro hizo, Rais alitoa siku moja ya jana kwa wakuu wa wilaya hizo na uongozi wa mkoa, wampatie takwimu kamili zikiwa na majina ya watu waliobomolewa nyumba ambao wanaishi kwa majirani na kambini, ili misaada inayotolewa iwafikie walengwa na si wajanja wachache ambao si walengwa.
“Uongozi unapimwa katika kipindi cha matatizo ya watu, sijaridhika na takwimu hizi, hazioneshi walengwa halisia... jipangeni vizuri mnipe taarifa kamili kesho (leo), ili Waziri William Lukuvi (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge) na wengine wazifanyie kazi kuwezesha upatikanaji wa huduma bila kuachwa mtu aliyeathiriwa na mafuriko,” alisisitiza.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, alisema watu 12,472 walikumbwa na mafuriko hayo na kaya 2,759 zimeathiriwa, wakati nyumba 1,141 zilibomolewa na nyingine 2,922 kuzungukwa na maji.

Alisema kuna mahitaji ya tani 635.5 za chakula kwa miezi sita kuanzia sasa na Sh milioni 57 kwa ajili ya kujenga makazi ya muda.

Wizara za Fedha, Elimu kuwekwa ‘kitimoto’

Zitahojiwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu matumizi ya marejesho ya fedha za radaDar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, PAC, imepanga kuzikutanisha kwa pamoja, Wizara za Fedha na Elimu wakati ikipokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayohusu matumizi ya fedha za marejesho ya rada jinsi zilivyotumiwa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deo Filikunjombe alisema kuwa wanatarajia kupokea taarifa hiyo kesho na watatumia fursa hiyo kujihakikishia kama matumizi hayo yalikuwapo au kama kulikuwa na ulaghai wa aina yoyote.
“Kwa sasa ni mapema kuanza kufikiri kwamba fedha hazikutumika inavyotakiwa, lakini kama kuna ujanja wowote ulifanyika tutabaini tu alisema na kuongeza:
“Ndiyo sababu katika kikao hiki tunakutana wote; CAG, Wizara ya Fedha na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kama kuna maswali basi kuwe na majibu yake papo hapo,” alisema Filikunjombe.
Alisema leo watapokea taarifa ya ukaguzi maalumu kuhusu mbolea ya ruzuku, pia shughuli nyingine ambazo kamati inatarajia kuzifanya katika kipindi cha wiki mbili zijazo ni pamoja na kutembelea bandari na kukagua mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe wilayani Ludewa.
Awali mwaka jana aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene, aliliambia Bunge kwamba fedha za rada zilizorejeshwa Sh72.3 bilioni ziliingizwa katika bajeti ya serikali kwa mwaka 2012/13.
Mbene alisema kwamba fedha hizo ni marejesho kwa Serikali ya Muungano kutokana na udanganyifu uliofanywa na Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza wakati wa kuiuzia Serikali ya Tanzania rada ya kuongozea vyombo vya usafiri angani.
Fedha zilizorudishwa na kampuni hiyo baada ya Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza kubaini kuwa, baadhi ya maofisa wa Serikali ya Tanzania na mawakala wa ununuzi kupandisha bei baada ya kushawishiwa na kampuni hiyo.
Novemba mwaka jana Serikali ilianza kusambaza vitabu milioni 19.4 kwa shule za msingi nchini, ambavyo ilielezwa kuwa vimenunuliwa kwa chenji ya rada na asilimia 75 ya fedha hizo zimetumika kununulia vitabu hivyo na asilimia 25 zitatumika kununulia madawati.

Vita ya umeme

WAKATI Watanzania wakilia ugumu wa maisha pamoja na mambo mengine, kupanda kwa gharama za nishati ya umeme, imethibitishwa kuwa kuna wafanyabiashara wanapambana bei hiyo isishuke. Wafanyabiashara hao; wenye mitambo ya kufua umeme wa mafuta na waagizaji wa mafuta, wananufaika kwa kunyonya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambalo linalazimika kuwapa karibu Sh bilioni nne kila siku, ili lipate umeme huo wa mafuta kutoka kwao.
Akizungumza juzi katika siku ya mwisho ya ziara yake ya kutembelea ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kuchakata gesi Mtwara na Lindi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema wafanyabiashara hao wanauzia Tanesco umeme uniti moja kwa kati ya senti 33 na 50 ya dola ya Marekani.
Bei hiyo ya umeme kwa Tanesco ni kubwa kuliko ambayo shirika hilo linauza kwa wateja wanaotumia umeme mdogo wa majumbani, wa kati kwa wafanyabiashara, wa kati viwandani na mkubwa kwa viwanda vikubwa, na kubwa kuliko bei ya umeme ya mashirika ya umeme ya nchi za Afrika Mashariki.
Tanzania kwa sasa inatumia megawati 1,850 ambazo asilimia 80 kwa mujibu wa Pinda, zinazalishwa kwa mafuta ya dizeli na mazito; wakati asilimia nyingine ndizo zinazotokana na vyanzo vingine vya maji na gesi ya Songosongo.
Bei ya umeme Kwa mujibu wa takwimu za Tanesco, wateja majumbani wananunua uniti moja kwa senti 19 ya dola, wateja wa biashara senti 13 na viwanda vya kati na vikubwa senti 10. Umeme wa taa za barabarani ni senti 19.
Kwa nchi za Afrika Mashariki, hasa Kenya, Uganda na Rwanda, wateja majumbani hununua uniti moja kwa senti 20, wa biashara ni kati ya senti 16 na 20.
Viwanda vya kati Uganda bei ni senti 17, Kenya 14 na Rwanda 19. Kwa umeme wa viwanda vikubwa, bei kwa Uganda ni senti 12, Kenya 15 na Rwanda 19. Tanzania inaongoza kwa kutoza bei kubwa kwa taa za barabarani ambayo ni senti 19 sawa na Rwanda huku Kenya na Uganda bei kwa umeme huo ni senti 18.
Hali hiyo inadhihirisha kuwa pamoja na kupandisha bei ya umeme mwezi huu, bado gharama za umeme kwa Tanesco ni kubwa kuliko bei ya kuuzia, na kusababisha shirika hilo muhimu katika uchumi wa nchi, kujiendesha kwa hasara.
Suluhisho Pinda alisema bomba la gesi kutoka Mtwara likimalizika kujengwa na uzalishaji kuanza, Tanesco itanunua umeme huo kwa senti 8 na kufanya nishati hiyo kushuka bei. Kauli hiyo ya kushusha bei ya umeme baada ya gesi kuanza kutumika Dar es Salaam, pia ilipata kutolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
“Hii bei ya umeme iliyopo sasa ni ya muda tu na itashuka sana bomba la gesi litakapokamilika, kwa sababu hata mitambo ya kufua umeme inayotumia mafuta nayo itatumia gesi na mitambo mipya ya gesi italetwa, nataka Watanzania wakubali hivyo.
“Serikali inataka umeme mwingi utokane na gesi, jua, upepo na joto ardhi, lakini wapo wanaokataa bomba kuja Dar es Salaam na hao hao wanalalamika umeme kuwa juu, mtu yeyote ambaye anajua dunia inakwendaje, hawezi kupinga kujengwa bomba la gesi.
"Miaka ijayo, chanzo kikubwa cha umeme nchini kitakuwa gesi asilia… nyie mtanitukana, mtanisema sana, lakini mimi nitabaki kwenye utaalamu na wala siwezi kuyumba, tatizo la umeme wa Tanzania litatatuliwa na gesi, kila kitu kikikamilika Tanesco na Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji) hawawezi kuendelea kuweka bei juu," alisema Profesa Muhongo.
Mapambano “Sisi tunaona kuwa suluhu ya kuondokana na gharama hizi ni gesi, lakini kuna watu wanajua watanyang’anywa tonge midomoni, vita hii tunaijua; lakini hatuwezi kurudi nyuma katika hili ni lazima tusonge mbele,” alisema Pinda.
Alisema nyuma ya mapambano ya kuzuia gesi kufika Dar es Salaam, wapo wafanyabiashara ambao wanahofia kuwa mwisho wa biashara yao ya kuuzia Tanesco umeme kwa bei ya juu umefika.
Alisema watu kwa sasa wananufaika na Tanesco kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme. Katika hali hiyo, Pinda alisema uamuzi wa Serikali kuchimba gesi hiyo na kuisafirisha hadi Dar es Salaam si jambo jepesi, kwani utekelezaji wake unakabiliwa na mapambano na upinzani mkubwa kutoka kwa wenye mitambo ya kuzalisha umeme ambao kwa sasa wananufaika kutoka Tanesco.
Alisisitiza, kuwa Serikali imedhamiria kuachana na umeme huo wa mafuta na kama wafanyabiashara hao wanataka kuendelea na biashara hiyo, ni vema wabadilishe mitambo yao iwe ya gesi na si ya mafuta kama ilivyo sasa.
Mataifa, ushauri Pia alisema vita nyingine wanayokabiliana nayo ni ya nchi ambako kampuni za utafiti wa mafuta na gesi zinatoka, ambazo zinataka kampuni zao zipewe zabuni ya kutandaza bomba la gesi na kujenga mitambo ya kuchakata gesi.
“Wanalalamika gesi wametafuta na kugundua wao, halafu kandarasi anapewa China, sisi tumewajibu kuwa tumekimbilia China kwa sababu masharti yao ni nafuu kuliko yao,” alisema Pinda.
Katika hatua nyingine, Pinda alitaka wakazi wa Lindi na Mtwara kutambua kuwa gesi hiyo ni rasilimali ya Taifa na itanufaisha nchi nzima. Aliwataka wajiandae kwa uchumi huo kwa kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo kufaidika. Aliwataka wasikubali fursa ya gesi ilete balaa nchini badala ya neema.
“Kama tunataka iwe neema tushirikiane na wadau wakubwa zaidi ili nchi yetu ipige hatua kimaendeleo.”
Kwa upande wake, Profesa Muhongo aliwataka wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kusomesha watoto wao hasa katika Sayansi, ili wafaidike na uwepo wa gesi na mafuta katika mikoa hiyo.
Alisema Serikali imejitahidi kusomesha vijana katika eneo la gesi na wamekuwa wanahamasisha vijana wa mikoa hiyo kuchukua masomo ya Sayansi kwa vile wizara inagharimia baadhi ya vijana kusoma masuala ya gesi vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi.

Pinda katika ziara hiyo alielezea kuridhika na kazi inayoendelea katika mradi huo na akasema upo uwezekano mradi huo ukakamilika kabla ya muda wake uliopangwa wa miezi 18.