MICHAKATO

Levis Rocky Ndekeno

Pages

Sunday, January 26, 2014

Waziri wa Fedha akiri hali ngumu

 Waziri wa Fedha, Saada Mkuya amekiri Serikali kuwa katika hali ngumu, lakini akasema kuwa mkakati uliopo ni kudhibiti matumizi ili yaendane na fedha iliyopo.
Waziri Saada alisema hayo kwa njia ya simu, alipotakiwa na Mwananchi Jumapili kujibu madai ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) juu ya kauli yake ya hivi karibuni aliyoitoa katika mkutano mjini Dodoma.
“Ni kweli nimesikia alichosema CAG na nadhani alimaanisha kudhibiti matumizi ya rasilimali kulingana na mahitaji. Siyo kwa Tanzania tu, nchi zote huwa zinazingatia matumizi ya rasilimali kulingana na mahitaji yaliyopo” alisema Saada na kuongeza:
“Sisi kama wizara tumejipanga kukusanya na kutegemea fedha zetu za ndani kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA). Tunategemea misaada, lakini huwa inachelewa. Hata wakaguzi nao wanapaswa kuangalia hilo.”
Hata hivyo, Saada alisema kuwa Serikali ina fedha za kutosha kuendesha shughuli zake.
Alhamisi wiki hii CAG,Ludovick Utoh akifungua Mkutano wa pili wa Baraza la Wafanyakazi wa Ukaguzi nchini mjini Dodoma alisema, Serikali ya Tanzania iko hoi kifedha hivyo Bunge na Serikali lazima wajitathimini na kuongeza wanayo matumaini kutokana na ushauri ambao umekuwa ukitolewa na ofisi yake kufanyiwa kazi.


0 comments:

Post a Comment