MICHAKATO

Levis Rocky Ndekeno

Pages

Tuesday, February 2, 2016

Brazil: Virusi vya Zika havitaathiri Olimpiki


Brazil Serikali ya Brazil imesema Michezo ya Olimpiki, inayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu, haitaahirishwa kwa sababu ya mlipuko wa virusi vya Zika.
Maafisa wa serikali wamesema hakuna hatari yoyote kwa wanariadha na mashabiki, ila tu kwa wanawake wajawazito.
Awali, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikuwa limeonya kuwa virusi vya Zika ni hatari kubwa kwa afya ya umma duniani na kutangaza hali ya tahadhari.
Shirika hilo limeyataka mataifa kuungana kuukabili ugonjwa huo.
Virusi hivyo vimehusishwa na kuzaliwa kwa watoto wanaozaliwa wakiwa na vichwa vidogo na ubongo uliodumaa
Wataalamu wameonya kwamba virusi hivyo vinavyoenezwa na mbu vinasambaa sana Amerika Kusini na kusababisha madhara makubwa.
"Lazima tuwafafanulie wale wanaojiandaa kuja Brazil, wanariadha, kwamba hawakabiliwi na hatari yoyote kama wewe si mwanamke mjamzito,” shirika la habari la Reuters limemnukuu msemaji wa Rais Dilma Rousseff, Jaques Wagner.

Rais Rousseff awali alikuwa ameidhinishwa wakaguzi wa afya na usafi kutumia nguvu, ikibidi, kufikia nyumba za watu binafsi, kama sehemu ya juhudi za serikali za kuangamiza maeneo ambayo mbu wanatumia kuzaana, hasa maji yaliyotulia.
Wakaguzi sasa wako huru kuitisha usaidizi wa polisi ikihitajika.
Zaidi ya wanajeshi 200,000 wanatumiwa kusaidia katika ukaguzi huo.
Wizara ya afya nchi humo imesema 25% ya nyumba 49 milioni nchini humo kwa sasa zimekaguliwa.

0 comments:

Post a Comment